Wafanyakazi kutoka True Vision Production (TVP) kabla ya kukabidhi sehemu ya msaada kwa wanafunzi wa shule ya msingi Jeshi la Uwokovu

Bagamoyo. Wanafunzi wa darasa la saba wa shule ya msingi ya Jeshi la Wokovu kwa watoto wenye ulemavu (Salvation Army Primary School for disabled and albino children), wamefurahia safari yao ya kwenda kutembelea sehemu za mji wa kihistoria Bagamoyo (Study Tour), ikiwa sehemu yao ya kujifunza kwa vitendo walichokisoma darasani kwa kipindi cha miaka 7 kabla ya kumaliza elimu yao ya shule ya msingi miezi michache ijayo.

David Sevuri wa TVP akimsaidia mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi Jeshi la Uwokovu wakati wa ziara yao mjini Kaole, Bagamoyo.

SOMA ZAIDI

Wakiambatana na wafanyakazi wa True Vision Production (TVP) waliofadhili safari hiyo, wanafunzi hao wamesema wamepata faraja sana kupata ufadhili wa safari hiyo.
Kilichowafurahisha zaidi ni wafanyakazi wa TVP kujumuika nao, kuwahudumia wale wenye ulemavu wa viungo na kula nao pamoja chakula cha mchana.

David Sevuri kutoka True Vision Production (TVP) akiwatia moyo wanafunzi wanaosoma shule ya mahitaji maalumu kwa wenye ulemavu wa kusoma kwa bidii ili waje kuwa watu wanaotaka baadae

Wakiongea kwa niaba ya wanafunzi wenzao, Noah Michael (15) amesema wamejifunza biashara ya utumwa ilivyoanza Pwani ya Afrika ya Mashariki, kikubwa zaidi akiwaomba TVP kuendelea kujitolea kwa wanafunzi wenye uhitaji.

“Tumejifunza mambo mengi, tumefurahia pia chakula kitamu, kikubwa zaidi TVP tumekuwa nao katika matembezi yetu, wametuletea chakula mezani na kuwa sehemu ya walezi wetu,” amesema Michael.

Wananfunzi wa shule ya msingi ya Jeshi La Wokovu wakimpongeza David Sevuri kutoka TVP kwa kuifadhili safari yao ya kwenda Kaole, Bagamoyo kujifunza kwa vitendo katika sehemu za kale.

Naye Joyce Mahona (14) , mwenye ndoto ya kuwa daktari, amesema amejifunza jinsi watumwa walivyokuwa wanauzwa, ameona msikiti wa kwanza kabisa kujengwa katika karne ya 13, kisima cha kale na kuona makaburi wa watu wa kale.
Alanus Lugome amesema mbali ya kuona vitu vingi vya kale, kikubwa zaidi kilichomshangaza ni kuuona mti wa ubuyu wenye miaka zaidi ya 500.

Mwalimu wa taaluma wa shule ya msingi Jeshi la Uwokovu, Anne Kibanga Mwamgunda amesema yeye, walimu wenzake na wanafunzi wao wamefurahi kujumuika na TVP katika siku muhimu kwao

Jane Mwabusila (Mama Angel) wa TVP akitoa msaada kwa mmoja wa watoto

Katika kudhihirisha ule usemi usemao ‘Disability is not Inability (ulemavu sio sababu ya kushindwa au kutojua kitu), wanafunzi hao walimshangaza mtembeza watu maeneo ya kale (Tour Guider), Leo Tagalile kwa maswali mazuri waliyouliza wanafunzi juu ya mji huo wa kihistoria.

Isaac Lukando na Nancy Sevuri walikuwa sehemu ya crew ya TVP kuwasaidia watoto wenye uhitaji maalumu.

Miongoni mwa maswali waliyoyauliza ni pamoja na kutaka kujua akina nani waliokuwa wenyeji wa eneo hilo kabla ya ujio wa wakoloni, kwa nini paliitwa Kaole na je mbuyu huo bado unatoa matunda licha ya kuwa na umri wa miaka 500?.
Pia wanafunzi hao, mbali na kuiona bandari ya kwanza katika Pwani ya Afrika ya Mashariki, pia walitembelea jengo la The Caravan Serai, lililojengwa mwaka 1870 kwa ajili ya kupokea watumwa waliotoka sehemu mbalimbali kama vile Kilwa Masoko kabla ya kuuzwa.

Mmoja wa wanafunzi kutoka shule ya msingi ya Jeshi la Uwokovu akiangalia moja ya vivutio ya vitu vya kale katika makumbusho ya Kaole.

“Mmefanya kitendo kikubwa sana kuwa nao na kufurahi nao kwa sababu wanafunzi wenye ulemavu wa viungo, huwa hawaamini kama jamii nyingine inawakubali na kuwathamini,”
“Siku zote wanajisikia faraja sana watu wengine wanapojumuika nao sababu wengine hata jamii  zao zinawatenga,”

Muongoza watalii, Leo Tagalile akieleza jambo kwa waliotembelea sehemu za kale za Kaole, Bagamoyo, mkoani Pwani

“Wao wamezoea kuwa karibu na jamaa zao na walimu wao tu, wakitokea watu wengine tofauti kama TVP na kuwa nao siku nzima, wao wanafarijika sana,” amesema Anne Kibanga Mwamgunda, mwalimu wa taaluma wa shule hiyo, inayojumuisha watoto wenye ulemavu wa viungo na ngozi (albino).
“Mbali ya kuwasaidia katika mitihani, pia itawapa kumbukumbu muhimu katika maisha yao,” amesema mwalimu Emmanuel Ibrahim.

Dickson George kutoka TVP akimsaidia mmoja wa wanafunzi wenye uhitaji kumuingiza katika basi wakati wa ziara yao ya kimasomo ya mambo ya kale.

Amesema mara ya mwisho wanafunzi wake kutembelea Kaole ni miaka miwili iliyopita kwa ufadhili wa aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP, marehemu Reginald Mengi.
Mmoja wa wafanyakazi wa TVP, David Sevuri amesema wamejisikia faraja kuwasaidia wanafunzi hao kwenda katika mji huo wa Pwani ya Bagamoyo kama sehemu ya kujifunza kwa macho, baada ya nadharia ya darasani.

Isaac Lukando (kushoto) na Dickson George wakishusha moja ya magunia kwa ajili ya kuwakabidhi watoto wenye uhitaji maalumu

“Tuliwahi kuwatumia wanafunzi watatu kutoka shuleni kwenu kutengeneza tangazo la televisheni la Haki Elimu, hivyo tukaona sababu nyingine ya kuwa karibu na nyinyi,”amesema Sevuri.
TVP, inayojihusisha na utengenezaji wa Makala maalumu za video (documentary) na matangazo ya radio, ilitoa pia magunia ya unga, mchele na mafuta kama sehemu ya msaada wa chakula kwa watoto hao.

Kapteni Sophia Jackson Myamhanga, ambaye ni matron (mlezi) wa wanafunzi wa shule ya msingi Jeshi la Uwokovu alikuwa sehemu ya msafara wa Kaole, Bagamoyo

Sehemu ya TVP crew wakijadili jambo kabla ya kujumuika na watoto wa shule ya Jeshi la Uwokovu