Kampuni ya True Vision Production (TVP) inatoa pole kwa Azam Media, tasnia ya habari, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia vifo vya wafanyakazi wake 5 waliofariki hivi karibuni katika ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Kizonzo, katikati ya Shelui na Igunga.
Waliofariki katika ajali hiyo ni pamoja na Charles Wandwi (Camera operator), Florence Ndibalema ( Sound Technician), Said Hassan (Camera Operator), Salim Mhando ( Vision Mixer) na Silvanus Kasongo ( Broadcasting Technician).
Mkurugenzi wa TVP, David Sevuri kwa masikitiko makubwa ameandika katika kurasa zake za mitandao ya kijamii na kurasa maalumu ya TVP, akielezea jinsi TVP ilivyoguswa na msiba huo, wakiwa kama wadau.
Katika ujumbe wake, Sevuri amesema
“Uongozi na wafanyakazi wa TVP wanatoa pole kwa uongozi na wafanyakazi wa Azam Media, kwa kuondokewa na wafanyakazi wenzao”Akielezea kuwa hilo ni pigo kubwa sana katika tasnia ya habari.
Sevuri pia ametoa pole kwa familia za wafiwa, ndugu na jamaa zao, huku akiomba Mungu awatie nguvu katika kipindi chote cha majonzi.
Viongozi mbalimbali, akiwemo Raisi John Pombe Magufuli wametoa salamu za pole kufuatia vifo hivyo. Wafanyakazi hao walikuwa safarini kuelekea Chato kwa ajili ya uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi, ambapo Raisi Magufuli alikuwa mgeni rasmi.
“Mungu azilaze roho za Marehemu Mahali pema Peponi”