Kampuni ya True Vision Production (TVP), kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na UNICEF, imeandaa semina ya siku tatu kwa wadau mbalimbali wa sekta ya afya, wakiwemo wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari, waandishi, viongozi wa dini na wadau wengine wa maendeleo ili kutoa elimu itakayopelekea kuhamasisha kushiriki katika kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’.
Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama ni kampeni ya Taifa, iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, mheshimiwa Samia Suluhu Hassan mjini Dodoma, mwezi Novemba mwaka jana, ukiwa ni mwongozo kutoka Wizara ya Afya kwa wakuu wote wa mikoa Tanzania Bara kuchukua hatua za kuzuia vifo vya mama na mtoto katika mikoa yao.
Madhumuni ya Serikali ni kuhamasisha viongozi wake, viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya serikali, wadau wa maendeleo, watoa huduma za afya, familia na jamii kwa ujumla kuanza kuchukua hatua za kuzuia vifo hivyo.
Moja ya malengo ya Kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ ni kupunguza vifo vya wanawake wajawazito, kutoka 556 mpaka 292, kama sio kumaliza kabisa ifikapo mwaka 2020.
Pia kampeni imeweka malengo ya kuokoa vifo vya watoto wachanga kutoka 43, mpaka 25 kwa vizazi hai 1,000 ifikapo mwakani.
Semina hiyo itaanza kesho (tarehe 22/04/2019) katika ukumbi wa Hoteli ya Regency, iliyopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam.
TVP ni waratibu wa semina hii ya siku tatu. Kwa mujibu wa mratibu kutoka TVP, Lilian Revocatus, maandalizi yamekamilika na tayari wadau wote wamepewa mialiko ya barua na wamethibitisha kushiriki.
Manguli wa sekta ya habari, wakiwemo Theophil Makunga, aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited na Abdalom Kibanda kutoka New Habari na akiwa kama mwenyekiti wa zamani wa jukwa la wahariri (TEF) ni miongoni mwa wengine wengi walioalikwa.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambazo zimekuwa zikipoteza mama wajawazito na watoto kutokana na matatizo yanayotokana na uzazi, licha ya jitihada zinazofanywa na serikali na wadau wengine wa katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya.
Ukosefu wa elimu ya afya, kukosekana kwa huduma muhimu, kama vile ukosefu wa hospitali, dawa za kutibu binadamu na vifaa tiba katika baadhi ya maeneno ni miongoni mwa sababu za vifo vitokanavyo na uzazi.
KWA MAELEZO ZAIDI BONYEZA HAPA