Suala la ukatili wa kijinsia bado limekuwa ni ajenda kubwa katika jamii ya Kitanzania lakini pia ulimwenguni kote. Matukio mbalimbali yanayoonyesha na kuashiria ukatili wa kijinsia yamekuwa yakiripotiwa na kukemewa na hata kuchukuliwa hatua kali na taasisi husika mara tu yanapojidhihirisha. Hii ni kusema kuwa Dunia bado iko macho katika kuangazia matukio kadha wa kadha ya ukatili wa kijinsia.
Shirika la TGNP mtandao kwa muda mrefu limekuwa likijitahidi kupambana na matukio hayo ya ukatili wa kijinsia. Na wakati mwingine kuhakikisha matukio haya hayajirudii tena katika jamii zetu. Mbinu na njia mbalimbali zinatumika katika kufikisha ujumbe kwa jamii kuepuka matukio hayo ukatili wa kijinsia.
Mkurugenzi mtendaji wa TGNP Mtandao Bi. Lilian Liundi akizungumza mbele ya washiriki wa Tamasha la 14 la jinsia lililofanyika mwishoni mwa mwezi Septemba amesema, tangu tamasha lianzishwe mwaka 1996, zaidi ya watu 30,000 wamefikiwa katika kusimamia na kupaza sauti pale TGNP inapoona mambo hayaendi sawa.
Amesema, TGNP inajivunia na imejidhatiti katika kuendesha harakati za kukomesha ukatili wa kijinsia katika kuhakikisha pamoja na mambo mengine, usawa unakuwepo kati ya wanawake na wanaume. Lakini pia TGNP inafanya kazi na mashirika/taasisi mbalimbali vikiwemo vikundi vya haki za binadamu katika kuzikabili sera zinazokandamiza wanawake hasa katika nchi maskini.
Tamasha la jinsia la 14 limefanyika mwishoni mwa mwezi Septemba, 2019 likibeba ujumbe unaosema “Wanaharakati wa kijinsia mbioni kubadilisha Dunia”. Tamasha ambalo lilienda sambamba na maadhimisho ya miaka 25 ya TGNP pamoja na azimio la mpango kazi wa Beijing uliokuwa na lengo la kupambana na ukatili wa kijinsia Duniani.
Tamasha la 14 la kijinsia 2019, liliudhuriwa na Mama Getrude Mongella, spika wa zamani wa bunge la Afrika, Spika wa zamani wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Anna Makinda, Naibu Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dr. Faustine Ndungulile, Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba, Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Anders Sjoberg pamoja na viongozi na wadau mbalimbali.